Nilipokutana na Yesu – Na. Rafik Daudjee
Nilizaliwa nikiwa mwamini wa Dini ya Kiislamu madhehebu ya Kibohora ya Dawoodi. Madhehebu hayo ni ya Ki-shia ambayo yalitokea nchini Yemen mnamo karne ya 10 na sasa yana makao yake makuu nchini India. Waumini wa madhehebu ya Bohora wanapatikana katika mabara kadhaa na miji mingi pote duniani.
Nililelewa katika mazingira ya kujifunza Kurani kwa kuhudhuria madrassa nikifuata Imani ya Ki-shia. Nilisoma Korani, nilisali na kufunga wakati wa mwezi wa Ramadhani. Imani ya msingi ya waumini wa madhehebu ya shia imejengwa juu ya ufia dini wa wajukuu wa mtume Muhammad ambao walikuwa ni Ma-khalifa halali waliostahili kuongoza dini ya Kiislamu lakini waliuawa katika vita ya Karbala.
Wakati nikiwa na umri wa miaka 16-17 hivi, nilishikwa na kiu kubwa maishani mwangu ya kutaka kumjua Mungu kibinafsi. Hivyo, nikaanza kuchunguza katika dini yangu nikitaka kuwa mcha mungu zaidi na mwenye ari kubwa zaidi katika Imani. Lakini, pamoja na hayo mimi niliandika katika kitabu changu cha kumbukumbu za kila siku siku zile “ewe Mungu uko wapi?” Hata hivyo, sikuweza kujiridhisha mimi mwenyewe na pia sikuweza kuwa na amani ndani yangu. Nilishikwa na wasiwasi na hofu kubwa kiasi kwamba sikuweza hata kutoka kwenda matembezini na kujumuika na marafiki.
Hapo ndipo nilipoanza kutafuta amani kupitia watu walioendesha Taamuli Mazingatio (Transcendental Meditation), Yoga na hata kujihusisha na ulimwengu wa Imani za mizimu na elimu ya ubashiri na kusoma nyota, lakini nilizidi kuchanganyikiwa na hakuna kilichoweza kunitosheleza. Nilikuwa mtu aliyerukwa na akili na mgonjwa sana na nikapatwa na mashambulizi ya taharuki ya hofu ya mara kwa mara.
Mwaka 1978, nilichaguliwa na serikali kufanya masomo ya kuwa Daktari Msaidizi ngazi ya Diploma mjini Mwanza, mji uliopo kwenye mwambao wa ziwa Viktoria. Wakati nikiwa katika mafunzo hayo na kutokana na mashambulizi hayo ya taharuki ya hofu, sikuweza kuwa mtulivu na kusoma na hivyo nikapelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu na nikapewa madawa makali yakiwemo ya usingizi kama vile Valium, Ativan, Librium ambayo niliyazoea na yakafanya usugu na nikalazimika kuongeza viwango vya matumizi yake. Niliweza kuendelea na mafunzo lakini sikuweza kupata amani ndani yangu na hivyo niliendelea kuishi maisha yenye hofu ingawa nilikuwa bado na kiu ya kuutafuta msaada kutoka kwa Mungu.
Siku moja Jumapili ya tarehe 17 mwezi Ferbruari mwaka 1980, wakati nikiendelea na mafunzo katika shule ya udaktari, ambapo ilikuwa ni miaka 10 hivi baada ya kumchumbia rafiki yangu mpenzi wa muda mrefu aliyeitwa Safia, nilikutana na Daktari mmoja ambaye alikuwa ni mkufunzi wangu na ambaye pia aliwahi kunitibu (wakati huo sikujua kuwa alikuwa Mkristo) siku ile alikuwa akizungumza kuhusu Sauli wa Tarso katika Kanisa dogo la pale chuoni. Akaniambia kama nitmnunulia kinywaji baridi aina ya Coca Cola, atanieleza kuhusu habari za “Sauli wa Tarso”. Tuliketi mgahawani naye akafungua Biblia yake katika Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura ya Tisa na kuniambia nisome kabla ya kutoa ufafanuzi (wakati ule sikujua huyu Sauli alikuwa nani wala sikujua ile sura niliyoisoma). Nilisoma aya ile na nikafika katika mistari hii ya sura ya 9:3 – 5 ya Kitabu cha Matendo ya Mitume:
“ Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza koto kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.”
Wakati nikisoma “Mimi ndiye Yesu”, niliomba kimya kimya, moyoni mwangu “Ee Mungu kuna ukweli wowote kuhusu huyu Yesu?” na katika wakati huo huo muujiza ulitokea ambao ulikuwa vigumu kuueleza. Nilijisikia kulipenda jina hilo na mvuto wenye nguvu sana ukatokea ndani ya moyo wangu kwa Biblia na jina la Yesu. Nikamuuliza yule Daktari “Mtu anawezaje kuwa Mkristo?”. Akaanza kunielezea mambo mengi kuhusu imani ya Kikristo lakini sikuweza kuyaelewa. Nilikutana na yule Daktari kwa mara nyingine tena wakati wa usiku naye akanieleza mambo mengi kutoka katika Biblia na kunitaka nisikilize ujumbe uliotolewa na Billy Graham. Ingawa sikuweza kuyaelewa yote niliyoambiwa lakini usiku ule jambo moja ninlilijua, Nilikutana na Yesu wakati nikisoma Biblia ile asubuhi ile. Siku iliyofuata asubuhi nikawa na kiu kubwa ya kusoma Biblia ndipo rafiki mmoja alinipatia Kitabu cha Agano Jipya kidogo cha kuweka mfukoni. Nikaanza kuisoma na kila neno ndani yake lilikuwa likizungumza nami. Nguvu, amani na furaha zikabubujika ndani ya moyo wangu wakati nikisoma, maandiko yalikuwa kana kwamba ujumbe wake ulikuwa umeandikwa mahsusi kwa ajili yangu pekee.
Maisha yangu yakaanza kubadilika. Sikuweza kuacha kuisoma Biblia. Nikaanza kumpenda Yesu, na Mungu akaingia ndani ya moyo wangu na tangu hapo nikaanza kuuona uwepo wake ndani yangu na nguvu ya Roho Mtakatifu. Baadaye niliponywa kimuujiza kutoka katika kuzoeleza matumizi ya dawa na nikafunguliwa kutoka nguvu za pepo wachafu. Baadaye Bwana aliniita niihubiri Injili. Unapomfuata Yesu, hufuati dini fulani. Yesu alikuja kutuokoa kutoka dhambi zetu. Kifo chake juu ya msalaba kilikuwa ni dhabihu ambayo Mungu aliitoa kwa ajili ya mwanadamu kwa ajili ya msamaha wa dhambi na kutuleta mahali pa kuwa na uhusuano wa binafsi na Mungu. Unapokutana na Yesu unaacha kuendelea kutafuta.
